MAHAFALI YA PILI YA CHUO CHA MANJANO BEAUTY ACADEMY YAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM
Wahitimu wa Chuo cha Urembo cha Manjano wametunikiwa vyeti katika nyanja ya urembo na vipodozi (Cosmetology). Baadhi ya wahitimu waliofika kwenye mahafali hayo walivikwa taji kama ishara ya mafanikio ya kitaaluma, na kuweka alama kwenye hatua muhimu katika maendeleo yao ya kitaaluma kwenye tasnia ya urembo na vipodozi. Zaidi ya wanafunzi 87 wamehitimu kwa mwaka huu wa 2018 na wataendelea na mafunzo ya utarajali (internship program) kwa kipindi cha miezi 12 katika masalon, kampuni na taasisi mbalimbali zenye kujihusisha na urembo na vipodozi ili kuweza kujijengea ujuzi (skills) na uzoefu (experience) katika kazi zao. Sherehe ilizinduliwa na Mkufunzi kutoka VETA, Mwl. Salehe Omari, akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, mama Florence Kapinga.
Mkuu wa Chuo cha Urembo mama Shekha Nasser akizungumza machache wakati wa mahafali ya pili ya Chuo cha Manjano Beauty Academy. Amewataka wanawake kujiongezea elimu ya matumizi sahihi ya Vipodozi na Urembo ili kuweza kutoa huduma sahihi na yenye ueledi kwa wananchi. Mama Shekha alisema Tanzania kuna upungufu mkubwa wa Wataalamu, hasa walimu wenye sifa za kufundisha elimu ya Urembo na Vipodozi, hivyo aliwashauri wanawake wengi kujiunga na Chuo cha Manjano Beauty Academy ili waendeleze tasnia hii na kuboresha huduma zao kwa wateja. Aidha alitaja changamoto kubwa alizokabiliana nazo wakati anaanzishi Chuo hicho ikiwemo ukosefu wa wataalamu wazawa wa maswala ya Urembo na Vipodozi. Akieleza zaidi alisema sekta ya urembo ina fursa kubwa kwa ajira na inaweza kusaidia kujiongezea kipato na kuondokana na ukosefu wa ajira na umasikini.
Mgeni rasmi, uongozi wa Chuo cha Manjano Bauty Academy na Wahitimu wakiwa katika picha ya pamoja.
Mgeni rasmi, Mwl. Salehe Omari, naye pia aliwashukuru wanawake wa Kitanzania waliojiunga kwenye chuo hicho kwa lengo la kupata ujuzi wa maswala ya urembo na vipodozi. Alisema Urembo, Vipodozi na mitindo ni moja kati ya sekta zinazoajiri mamilioni ya wanawake kwa sasa, na kuchangia kwa kiasi kwenye pato la Taifa. Akiendelea zaidi alisema, elimu na mafunzo kwa vitendo (Vocational training) ni elimu na mafunzo ambayo yanayotoa ujuzi na elimu muhimu kwa ajili ya ajira. Elimu ya aina hii ni ambayo humuandaa mtu kufanya kazi katika fani mbalimbali, kama biashara, utengenezaji wa vitu, au kama fundi. Hivyo aliwausia wahitimu kuitumia vizuri elimu na ujuzi walioupata kwenye Chuo cha Manjano. Alielezea pia kwa kusema elimu ya ufundi na ujuzi ni muhimu katika kuleta usawa kwenye jamii kwani ni moja ya kitovu cha kuleta maendeleo na kuendana na kasi ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda. Elimu ya ufundi, stadi za kazi au wa kazi za mikono ni mojawapo ya vipaumbele vya UNESCO. Kwani elimu hii inasaidia kuendeleza elimu ya ubora na usawa na fursa za kujifunza kwa wakati wote ule haijalishi umri wako, “wewe ni mwanafunzi wa kudumu alisema.”
Tunawatakia wasomi wetu wote kila la kheri katika kazi zao. Mkuu wa Chuo cha Urembo Mama Shekha Nasser akizungumza.
Shekha ni mmiliki wa kampuni ya Shear Illusions na mnamo mwaka 2015, kupitia bidhaa za LuvTouch Manjano alianzisha chuo cha Manjano Beauty Academy kwa lengo la kutoa elimu na ujuzi wa kuwawezesha wasichana na wanawake kujiajiri na kujiongezea kipato kupitia tasnia ya Urembo na Vipodozi.
0 comments: